MAJUKUMU YA VIONGOZI WA MTAA

 

MSAIDIZI WA MCHUNGAJI:

(01)Atasaini barua zote zinazomhusu mchungaji wa mtaa anapokuwa hayupo na kuendesha majukumu yote ya kichungaji isipokuwa kubatiza na kufungisha ndoa.

(02) Atawasiliana na ofisi ya konferensi kupata mchungaji wa kuendesha huduma ya ubatizo na ndoa kwa agizo la mchungaji au wakati mchungaji anapokuwa hayupo.

(03) Atapokea wageni wote wa mtaa na kuwapatia huduma zote zitakazohitajika kwa niaba ya mchungaji wakati mchungaji anapokuwa hayupo.

(04) Ataendesha vikao vya mtaa mchungaji asipokuwepo au anapoagizwa kufanya hivyo na mchungaji.

(05)Atasaidiana na katibu wa mtaa kuhakikisha fedha ya matumizi ya ofisi ya mchungaji inapatikana kwa wakati na kazi zilizokusudiwa hazikwami.

(06)Atasaidiana na katibu wa mtaa kuhakikisha taarifa za kila mwezi na kila robo zinaandaliwa na kutumwa konferensi kwa wakati.

(07)Atasaidiana na mkuu wa kambi na katibu wa mtaa kuhakikisha kamati za kambi zinatimiza wajibu wake na kuona kambi linafanyika kwa utulivu na mafanikio makubwa.

 

KATIBU WA MTAA:

(01)  Atakuwa mtendaji mkuu wa shughuli za siku kwa siku za mtaa akishirikiana na mchungaji wa mtaa ama msaidizi wa mchungaji wa mtaa wakati mchungaji anapokuwa hayupo.

(02)  Atahakikisha ofisi ya mtaa inakidhi viwango wakati wote kwa kutunza nyaraka nyeti za kiofisi na vitendea kazi muhimu ili kutokwamisha huduma zozote za kiofisi.

(03)  Atawapa taarifa wajumbe juu ya kuwepo kwa kikao cha mtaa na ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa, na kuandika kumbukumbu za vikao vyote vya mtaa.

(04)  Atatunza kumbukumbu za vikao na nakala za barua nyingine za ofisi ya mchungaji zitokazo katika ngazi za juu.

(05)  Atapokea na kukagua taarifa za fedha ziendazo konferensi na kukatia risiti baada ya kuzikagua na kuridhika nazo.

(06)  Ataandaa taarifa ya fedha ya pamoja ya mtaa na kuiwasilisha kwa mchungaji kabla ya siku ya kutuma taarifa au kuiwasilisha kwa wakusanya taarifa siku ya taarifa.

(07)  Atatunza nakala za taarifa za mtaa zinazotumwa konferensi kwa mwezi na kwa kila robo

(08)  Atasimamia makundi ya WhatsApp ya mtaa na kuthibiti matumizi yasiyo sahihi.

(09)  Atatoa matangazo ya mara kwa mara kwa wadau wote kwa kadri yatavyohitajika na kwa kadri atakavyokuwa akiyapokea kutoka kwa mchungaji. 

 

MKUU WA HUDUMA WA MTAA:

(01)  Atahimiza wakuu wa idara kutuma taarifa kwa wakati na kutoa usaidizi wa namna ya kuzijaza pale inapohitajika.

(02)  Atasimamia mkakati wa uongoaji roho (effort) wa mtaa au wa kikanda uliopo, na kupendekeza bajeti husika na kamati mbalimbali za mkakati huo.

(03)  Kuunganisha mapendekezo ya bajeti za kamati mbalimbali za makambi na kushauriana na mchungaji na katibu wa mtaa juu ya namna bora ya kufanikisha makambi hayo.

(04)  Ataratibu ratiba ya wahubiri wa mtaa watakaokuwa wakitoa huduma makanisani kwa mzunguko wa robo akisaidiana na mchungaji na katibu wa mtaa.

(05)  Ataandaa na kutunza fomu za taarifa zote zitakazohitajika kila mwezi na kila robo naye atazigawa kwa wahusika na kuwasaidia kuzijaza wale wasioelewa namna ya kuzijaza.

(06)  Atahimiza utumaji wa taarifa za mwezi na za robo kwa wakati kutoka kwa wakuu wa Idara ama viongozi wengine wa makanisa ya mtaa.

(07)  Atawatumia wahusika ratiba ya utumaji wa taarifa ya kila mwezi na kuwahimiza kuzingatia muda wa kuzituma.

 

MRATIBU WA MUZIKI:

(01)  Ataratibu na kuvisimamia vikundi vya uimbaji katika mikusanyiko inayofanyika kimtaa.

(02)  Ataratibu makongamano ya kwaya na makongamano ya vikundi vya uimbaji kimtaa kwa lengo la uinjilisti, kusifu na kujinoa kitaaluma.

(03)  Ataratibu mafunzo ya utaalamu wa muziki au kuwahimiza kujiunga na mafunzo ya muziki, walimu wa kwaya, wahudumu wa nyimbo za vitabuni, wanakwaya na waimbaji kutoka vikundi vya uimbaji vilivyosajiliwa makanisani.

(04)  Ataratibu Kwaya ya pamoja ya mtaa katika matukio ya kimtaa.

(05)  Atasimamia uandaaji wa bajeti ya muziki kwenye makambi ya mtaa.

 

MRATIBU WA HUDUMA ZA WANAWAKE:

(01)  Ataratibu na kuhamasisha ushiriki wa wanawake wa mtaa kwenye semina, na makongamano ya kimtaa na ya ngazi za juu ya wanawake.

(02)  Ataratibu na kuandaa mafunzo ya wanawake wa mtaa kwa kuwaalika wawezeshaji mbalimbali waliobobea katika fani na taaluma zenye changamoto kwa wanawake.

(03)  Atasaidia kutambulisha huduma ya wanawake makanisani ili kuongeza uelewa na uungwaji mkono wa huduma hii.

(04)  Ataratibu namna ya kuwasaidia wanawake wenye changamoto na watu wengine wenye mahitaji maalumu walio kwenye jamii tunayoishi.

(05)  Atasaidia kuanzishwa kwa jumuiya ya wajane wa mtaa na kushirikiana naoi li kuona changamoto zao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

(06)  Ataratibu mkutano wa injili utakaoendeshwa na wanawake ili kuimarisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za ushuhudiaji na uongoaji wa roho.

 

KIONGOZI WA MAJENGO:

(01)  Atasimamia miradi yote ya ujenzi ya kimtaa na kuikamilisha kwa wakati.

(02)  Atapendekeza bajeti ya miradi mbalimbali ya ujenzi ya kimtaa na kuiwasilisha kwenye vikao vya mtaa.

(03)  Kwa kutumia kamati ya ujenzi ya mtaa atakayoiunda na kwa ushawishi wake, atatafuta wafadhili wa ndani na nje wa kusaidia kukamilisha miradi ya ujenzi ya mtaa iliyopo na inayokusudiwa kuzinduliwa.

(04)  Atahimiza upatikanaji wa hati za viwanja vya makanisa ya mtaa, na kuona namna ya kuyasaidia makanisa yaliyo kwenye migogoro ya ardhi ili kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa viwanja vyenye migogoro.

(05)  Atasaidia upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kwa gharama nafuu kupitia msamaha wa kodi na punguzo la bei kutoka kiwandani.

(06)  Atasimamia ukamilishaji wa mradi wa nyumba ya mchungaji na ofisi ya mtaa.

 

MRATIBU WA VIJANA:

(01)Kwa kushauriana na viongozi wa kanda, ataratibu mikutano ya injili kimtaa inayoendeshwa na vijana.

(02) Ataratibu mafunzo ya wahubiri vijana kwa kutumia wakufunzi wabobezi.

(03) Kwa kushirikiana na viongozi wa kanda, atawahimiza vijana kuhudhuria mikutano, makongamano, na makambi ya vijana vilivyoitishwa na ngazi za juu.

(04) Ataratibu makongamano na mikutano ya vijana wa mtaa

(05)Kwa kushirikiana na viongozi wa kanda, ataratibu matendo ya huruma ya kimtaa ya vijana.

(06) Kwa kushirikiana na viongozi wa kanda atasaidia kuinua kanisa lililo nyuma katika shughuli za vijana.

 

MRATIBU WA WATOTO:

(01)Kwa kushauriana na viongozi wa kanda, ataratibu mikutano ya injili kimtaa inayoendeshwa na watoto.

(02) Ataratibu mafunzo ya wahubiri watoto kwa kutumia wakufunzi wabobezi.

(03) Kwa kushirikiana na viongozi wa kanda, atawahimiza watoto kuhudhuria mikutano, makongamano, na makambi ya watoto vilivyoitishwa na ngazi za juu.

(04) Ataratibu makongamano na mikutano ya watoto wa mtaa

(05) Kwa kushirikiana na viongozi wa kanda, ataratibu matendo ya huruma ya kimtaa ya watoto.

(06) Kwa kushirikiana na viongozi wa kanda atasaidia kuinua kanisa lililo nyuma katika shughuli za watoto.

(07)Atapendekeza  wahudumu wa watoto kwenye makambi ya mtaa na kuwasimamia ili kuona wanafundisha kulingana na miongozo iliyotolewa..

 

MRATIBU WA SHULE YA SABATO:

(01)  Ataratibu Shule ya Sabato inayohitimisha makambi ya mtaa.

(02)  Ataratibu na kuendesha Shule ya Sabato kwenye makambi ya mtaa.

(03)  Ataratibu semina ya mtaa ya viongozi wa Shule ya Sabato.

(04)  Ataratibu semina ya uendeshaji wa vipindi vya majadiliano ya lesoni redioni.

(05)  Atahimiza makanisa na washiriki katika kuendesha mijadala ya lesoni.

(06)  Atasimamia group la Whatsap la Shule ya Sabato ya mtaa ambapo taarifa mbalimbali muhimu na majadiliano juu ya namna ya kufakisha majuku ya idara yatakuwa yakifanyika.

 

MHAZINI WA MTAA:

(01)  Ataandaa taarifa ya fedha ya mtaa ya kila mwezi, kila robo na ya mwishoni mwa mwaka, ikionesha makanisa yalivyotoa fedha ziendazo Konferensi na zinazobaki makanisani.

(02)  Ataandaa taarifa akionesha uwiano wa kilichotolewa na kilichotarajiwa kwa mujibu wa magoli ya kila kanisa na ya mtaa kiasi kilichopungua kufikia lengo.

(03)  Ataandaa taarifa akionesha watoao kwa mpango, watoao zaka tu na wasiotoa kabisa kwa kila kanisa ili kuainisha wanaofanya vizuri katika maeneo hayo na wanaohitaji msaada.

(04)  Ataandaa taarifa akionesha kipato cha washiriki wa makanisa kwa mujibu wa matoleo yao (per capita) akiainisha wale wanaofanya vizuri na waohitaji msaada.

(05)  Ataandaa taarifa ya mwitikio wa magoli ya sadaka za kambi na michango ya kambi akiainisha kanisa linalofanya vizuri na wale wanaohitaji msaada.

(06)  Ataandaa taarifa akionesha mwitikio wa michango ya ofisi ya mchungaji na michango ya ukamilishaji wa nyumba ya mchungaji wa Mtaa, akiainisha kanisa linalofanya vizuri na lile linalojikongoja.